Prof. Masumbuko Lamwai
1. Dokta Masumbuko ndiye mtanzania wa kwanza kutunukiwa Shahada ya udaktari wa Falsafa katika sheria (PhD/LLD in Criminal and Procedural Law) kutoka Chuo Kikuu cha Oxford, moja ya vyuo vikuu vinavyoheshimika sana duniani.
2. Ndiye mwanafunzi wa kwanza kutoka barani Afrika katika chuo hicho kusoma kozi ya miaka minne kwa miaka miwili. PhD in Criminal and Procedural Law, chuo kikuu Oxford ni miaka minne (full time) na miaka 6 hadi 8 (part time). Lakini Lamwai aliomba kusoma kwa miaka miwili na akafaulu vizuri.
3. Mwanzoni mwa miaka ya 1990 akiwa Mhadhiri chuo kikuu cha Dar es Salaam alishirikiana na wanaharakati wenzie kuanzisha vuguvugu la kudai mfumo wa vyama vingi nchini.
4. Ndiye diwani wa kwanza na wa pekee wa upinzani Dar es Salaam. Mwaka 1994 aligombea udiwani Kata ya Manzese kupitia NCCR Mageuzi. Alishinda lakini CCM wakachakachua. Akaenda Mahakamani kudai haki yake. Mahakama ikabatilisha matokeo. Uchaguzi ukarudiwa, akagombea na kushinda. Leo vyama vya upinzani vina mamia ya madiwani lakini Lamwai ndiye aliyefungua njia.
5. Akiwa diwani pekee wa upinzani kati ya madiwani zaidi ya 20 wa CCM Manispaa ya Kinondoni aligombea Umeya na kupata kura moja (ya kwake). Alipoulizwa kwanini aligombea wakati alijua hatashinda, alijibu “nisingegombea ningelazimika kumpa mgombea wa CCM au kuharibu kura yangu. Yote mawili si sahihi. Hivyo niliamua kugombea ili nimpe kura mgombea anayefaa”
6. Ndiye Mbunge wa kwanza na wa pekee wa upinzani jimbo la Ubungo baada ya kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka 1995.
7. Ndiye mbunge aliyebadilisha kiapo cha wabunge. Akiwa bungeni alikataa kuapa baada ya kuona kiapo kinaelekeza Utii kwa Serikali. Akasema wabunge hawapaswi kutii Serikali kwa sababu bunge ni mhimili unaojitegemea. Baada ya mabishano makali ya kisheria, hatimaye Spika Msekwa alikubaliana na hoja yake. Kiapo cha wabunge kikafanyiwa marekebisho na kuondoa sehemu ya “utii kwa Serikali” kisha wabunge wote wakaapa upya maana wengi walikuwa tayari wamekwisha kuapa na kiapo kikawa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
8. Mwaka 1996 aliongoza kesi maarufu ya uchaguzi iliyomvua ubunge aliyekua Mbunge wa Temeke, Ramadhani Kihiyo kutokana na kughushi taarifa kuhusu elimu yake. Mbali na kesi ya Kihiyo ameshiriki pia kusimamia kesi mbalimbali nje na ndani ya nchi. Mwaka 2006 alishiriki kuandaa muongozo wa Haki za binadamu kwa nchi za jumuiya ya madola.
9. Mwaka 1999 baada ya kupitia misukosuko mingi ya kisiasa ikiwemo mali zake kupigwa mnada, kufilisiwa na kufutiwa leseni ya uwakili aliamua kurudi CCM.
10. Dr.Masumbuko Lamwai ni kaka yake Mhe.Joseph Selasini (Mbunge wa Rombo). Majina yake kamili ni Dr. Masumbuko Romani Mahunga Lamwai.